Na Kiranga
Nimekuwa nikifuatilia habari ya vazi la taifa kwa zaidi ya mwaka sasa. Mwanzoni kabisa nilifikiri ni habari ya waandishi kuongeza chumvi kwa kutaka kuuza magazeti, maana haikuniingia akilini kwamba kwa muda huu na matatizo yote yanayotukabili kweli kuna “kiongozi” anayeweza kuweka vitu katika mizani atataka kujishusha kwa kudakia kisicho kipaumbele. Nikajiuliza, lakini tangu lini viongozi wetu wa sasa wakategemewa kuweka vitu katika mizani? Nikataka uhakika zaidi.
Kukaja kauli, kamati, vikao vyenye ushahidi wa picha zilizosherehekewa, na mpaka vitisho vya ki-Augustine Mrema vilivyotoka kutoka kwa Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr. Emmanuel Nchimbi, kuhusu umuhimu wa kumaliza mchakato huu wa “kutafuta” vazi la taifa. Nikaona hakuna sababu ya kuendelea kunyamaza, hata kama ni kwa kuonesha dunia na Watanzania wenzangu tu kwamba kazi tunaijua na kanyaboya tunaijua tukiiona hata maili elfu kumi.
Kwa nini naliita zoezi hili kanyaboya? Ni zoezi lililojikita zaidi katika kuonesha serikali inafanya kazi, kuliko katika kufanya kazi yenyewe. Halina uhalisi. Ni hadaa ya wazi ikimbiliayo kututusi. Napata tabu kuelewa kijana anayejitambulisha na usomi kama Dr. Nchimbi, ambaye tungetegemea apeleke nguvu mpya serikalini kwa kutetea ushirikishwaji moja kwa moja wa wananchi, bila mazingaombwe ya kamati za kiimla ziso tamati, anakuwa mshabiki wa kuiongezea serikali kazi ya kupaka rangi nyumba bila kurekebisha msingi wa nyumba unaodidimia kwa nyufa.

22.12. 2011. Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dr. Emmanuel Nchimbi akizundua kamati maalum ya kutafuta Vazi la Taifa. Picha na Francis Dande; issamichuzi.blogspot.com
Waziri anahamanika na vazi la taifa wakati wananchi hawana hata mavazi? Seuze la taifa! Swala zima la “Vazi la taifa kwa kamati ya kiserikali” linanuka utawala wa kiimla unaokusudia kutuma ujumbe kipropaganda kwamba “wananchi hamuwezi kupata vazi mkalienzi wenyewe mpaka msaidiwe na serikali”. Ni tusi kwa mtu anayefikiri. Mi’ si mpinga serikali kwamba niseme serikali haitakikani. Kuna masuala makubwa, magumu, yanahitaji kusimamiwa na serikali.
Mathalani, hususan kwetu huku, hatujafikia kiwango cha uchumi wa kusema watu binafsi watasimamia mtandao wa barabara. Inabidi serikali ilipwe kodi, nayo itumie kodi kuimarisha miundombinu kama barabara. Ingawa hata hili nalo kuna mabepari wa soko huria wanaweza kutaka liachwe kwenye nguvu za soko, lakini hata nchi zilizoendelea tunaona serikali zinasimamia hili. Kwa hiyo, yapo mambo haya. Sipingi serikali kufanya kazi yake pale inapotakiwa. Lakini vazi la taifa? Baada ya hilo tutataka serikali itupangie nini tena? Chakula? Maana waziri wa afya anaweza kusema Watanzania tunahitaji kula mboga fulani kila Alhamisi ili kudumisha afya.
Nani ni mtoto hivyo kuhitaji kuvishwa? Vazi gani la taifa ambalo halihusiki na propaganda za kisiasa litatoka katika kamati ya kiserikali? Tayari kwa kufanya vazi la taifa jambo la kamati ya kiserikali, wamelitia doa la siasa jambo la kiutamaduni. Watu wengine wataanza kuangalia “kamati yenyewe yumo nani?” Mmiliki wa redio inayokuwa karibu sana na chama tawala? Mambo ya kutuzuga tu na kutengeneza ukondoo kwa wananchi na mianya ya rushwa. Sina nia ya kupanda mbegu ya kugawanya watu, lakini kuna matatizo mengine tunaweza kuyaona hivi hivi watu wanayapalilia bila sababu.
Kama leo wakisema “vazi la taifa hili hapa”, kesho nini kitawazuia kusema “na duka mtakalonunulia hili hapa”, na keshokutwa tunarudishwa enzi za Mfalme Jean-Bédel Bokassa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kuambiwa “wanafunzi wote mtabadili sare zenu na shurti mnunue duka la bwana mkubwa mmoja”. Au enzi za kamanda Thomas Sankara aliyekuwa akifanya ukaguzi mwenyewe ofisi za serikali kuhakikisha wafanyakazi wa serikali wanavaa “vazi la taifa”. Lakini angalau Sankara alikuwa mchuuzi wa “nchi ya kufikirika” aliyekuwa na mada ya kutaka viwanda vya kwao vishone nguo zaidi, sio watu washabikie mitumba ya California tu. Nchimbi wetu anahubiri vazi la taifa bila kufufua viwanda, sijui tutaliagiza kutoka Pakistani?
Najua unaweza kusema napeleka mambo mbali, lakini dhima hii ya kupumbaza wananchi kwa umangimeza uliojaa imla ni ile ile ya Bokassa tu, wafanye watu wajione wanyonge na hawawezi hata kile kidogo ambacho wanaweza, kisha badala ya kufanya kazi muhimu kama kushughulikia ubora wa pamba yetu, na kufufua viwanda vya nguo pamoja na kuhuisha vikundi vya mafundi washoni kwa kuwezesha mazingira ya mikopo nafuu (kazi nzito ya serikali), tafuta mazingaombwe yasiyo mwanzo wala mwisho kama kamati ya “Vazi la Taifa”.
Tunashuhudia ukoloni ukirudi upya. Ukoloni ambao ni mgumu sana kuung’amua kwa sababu mkoloni sasa si Muingereza, ni mweusi mwenzetu. Badala ya kutuambia “kibwaya chako ni vazi la kishenzi, vaa suti”, mkoloni huyu wa leo anatuambia “wewe huwezi kuchagua vazi zuri, tuachie sie watawala wako tukupangie”. Hiyo habari nzima ya kwamba kamati itatafuta vazi halafu litapelekwa kwa wananchi ni kutafuta mzozo tu, na kwa kweli inanikumbusha hukumu za sinema za “cowboys” wa zamani Magharibi ya Marekani ambapo watu wanakubaliana kumnyonga “mhalifu” kwanza, halafu kabla ya kumnyonga wanajidai kumpa tia nafasi ya hukumu ya haki.
Watu wakikaa kimya si kama hawaoni viongozi wanavyotapatapa kwa kushindwa kufanya la maana katikati ya utajiri wa umasikini. Hasha, pengine wanawavutia pumzi mlitangaze hilo vazi la taifa walichomelee moto mbali. Mtu hana chakula, dawa, elimu, mavazi wala matumaini yoyote katika maisha, unamwambia habari za vazi la taifa? Si ataona unamtukana? Na ukisema sio lazima wote wawe nalo hilo vazi, je litakuwa “vazi la taifa” kweli? Au tunataka kurudishana kwenye propaganda za kuuma na kupuliza kama Mobutu Sese Seko na sera zake za danganya toto kwa kisingizio cha “Uafrika”?
Nchimbi na kamati ya mazingaombwe, wingu la “vita baridi” lishaisha, ukungu umetoka machoni pa watu. Mnapofanya kazi kweli tunaona, mnapotapatapa kujionyesha mnafanya kazi kama mtu anayechafua meza kwa makaratasi bila kufanya la maana tunaona. Kama mna nia ya kweli kupata vazi la taifa vunjeni kamati, rudini kusuka mpango wa kufufua viwanda vya nguo na kuweka mazingira ya mafundi ushoni wadogo wadogo pamoja na wanamitindo wetu kuweza kufaidika kwa kushona nguo nchini. Wananchi wanaweza kuchagua wenyewe. Hawakuhitaji kamati wala kikao kuvaa khanga na vitenge, vikoi na migolole. Hizi habari za “vazi la taifa kwa kamati” zinaleta maswali mengi kuliko majibu, mwishowe mtaona aibu bure kwa kutaka kuturudisha mwaka 1984 wakati jini la muamko wa kisiasa lishatoka katika chupa ya “chama chashika hatamu”. Wengine tushajua viongozi wamegeuka watawala, watawala wakageuka wa-twawala, na “chama chashika hatamu” kimegeuka “chama chashika patamu”.
Kama Mwalimu Nyerere, aliyekuwa na kazi ya kulijenga taifa hili, kipenzi cha wengi, aliyetawala bila televisheni ya kuonesha watu vibikini vya Hollywood bali RTD iliyojaa “Mazungumzo Baada ya Habari” ya Abdul Ngalawa, MWATEX bila mitumba, magazeti ya Uhuru na Mzalendo bila tovuti za ukosoaji na TANU/CCM bila chama cha upinzani, alishindwa au hakutaka kuwepo vazi la taifa, nini kinafanya viongozi wa Tanzania ya leo waamini kwamba vazi la taifa la kuamuliwa na serikali ni jambo jema na linawezekana? Au Waziri wa Vijana , Michezo na Utamaduni hajui methali ya Kiswahili isemayo, “Samaki mkunje bado mbichi, akishakauka hakunjiki”? Je kasikia “Fupa lilomshinda fisi mbwa hataliweza”?
* * *
Ndugu msomaji, una maoni gani? Je, Watanzania tunahitaji Vazi la Taifa? La kuchaguliwa na kamati maalumu ya serikali?
Makala zaidi kutoka kwa Kiranga: